Historia, sababu na Hati za Muungano Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
iliundwa
mnamo tarehe 26 Aprili 1964 kwa
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar
inayojumuisha
Visiwa vya Pemba na Unguja 27/05/2009
HISTORIA YA MUUNGANO WA TANGANYIKA
NA ZANZIBAR
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
iliundwa mnamo tarehe 26 Aprili,1964 kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar
(inayojumuisha Visiwa vya Pemba na Unguja). Tanganyika ilikuwa ni mwendelezo wa
koloni la Ujerumani, utawala wa Waingereza kwa Mamlaka ya Umoja wa Mataifa,
Himaya ya Umoja wa Mataifa chini ya utawala wa Uingereza na mwisho Taifa huru
kuanzia mwaka 1961 ndani ya nchi za Jumuiya ya Madola. Jamhuri ya Tanganyika na
Jamhuri ya Watu wa Zanzibar ziliingia mkataba wa Muungano mnamo mwaka 1964 na
kuanzishwa Dola ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mkataba huu wa Muungano
ulitiwa saini na aliyekuwa Rais wa
Tanganyika, Hayati Mwalimu Julius Nyerere na aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Hayati
Sheikh Abeid Amani Karume tarehe 22 Aprili 1964 huko Zanzibar. Mkataba huo ulithibitishwa
na Bunge la Tanganyika na Baraza la Mapinduzi hapo
tarehe 26 Aprili, 1964 na mnamo
tarehe 27 Aprili, 1964, viongozi wa nchi zote mbili walikutana katika ukumbi wa
Karimjee Jijini Dar es Salaam na kubadilishana Hati za Muungano. Sheria za
Muungano zilitoa tamko la Jamhuri ya Muungano katika Ibara ya 4 kwamba:
“Jamhuri
ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar zitalazimika,
baada
ya kuungana na siku zote baada ya kuungana, kuunganishwa
kuwa
Dola ya Jamhuri kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika
na
Zanzibar’ (Ibara ya 4 Sheria za Muungano)
Jina hili la “Jamhuri ya Muungano wa
Tanganyika na Zanzibar” lilibadilishwa baadae mnamo tarehe 28 Oktoba, 1964 na
kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kupitia Sheria ya Jamhuri ya Muungano,
Sheria namba 61 ya mwaka 1964.
Watanganyika kama ilivyokuwa kwa
wananchi wa nchi nyingine zakiafrika, hawakukubaliana hata kidogo na utawala wa
kikoloni. Tangu mwanzo waliwapinga na kupigana na wavamizi wa kikoloni,
upinzani mkubwa ukionyeshwa na Wasambaa wakiongozwa na Kimweri dhidi
ya Wajerumani, Wahehe wakiongozwa na
Mkwawa kupigana vichungu na virefu dhidi ya Wajerumani na wakati wa vita vya
Maji Maji chini ya uongozi wa Kinjekitile, Mputa na Kibasila.
Kukosekana kwa umoja kati ya
wapigania uhuru hawa wa mwanzo na uimara wa majeshi ya wakoloni na silaha bora
za moto kulidhoofisha mapambano haya ya uhuru na kusababisha hasara kubwa na
kupoteza maisha ya watu.
Kama ilivyokuwa kwenye makoloni
mengi ya Kiafrika, hisia za Utaifa ziliendelea kuimarika katika Tanganyika
baada ya mwaka 1945. Alama za utaifa zilishaanza kuonekana punde baada ya vita
kuu ya kwanza ya dunia kwa kuanzishwa kwa vyama mbalimbali vya
Waafrika kwa upande wa Tanganyika na
Zanzibar. Kwa upande wa Tanganyika, African Association ilianzishwa mwaka 1929
kama kikundi cha mijadala baina ya wasomi na ilipofika mwaka 1948 chama hiki
kikawa Tanganyika African Association (TAA).
Baada ya vita ya Pili ya Dunia,
wanachama wa Tanganyika African Association mwaka1957 na kuunda chama kilichoitwa Afro-
Shirazi Union ambacho baadae kiliitwa Afro-Shirazi Party chini ya uongozi wa
Sheikh Abeid Amani Karume. Mwalimu Nyerere alishiriki katika mkutano huu.
Ilikuwa tarehe 05 Desemba, 1957 hapo mtaa wa Mwembekisonge Unguja.
Kati ya mwaka 1957 mara tu baada ya
uchaguzi mkuu wa kwanza na mwishoni mwa mwaka 1963, kabla ya mapinduzi ya mwaka
1964, Zanzibar ilitawaliwa na vuguvugu na mivutano mikali ya kisiasa. Mapambano
haya ya kisiasa yalikuwa kati ya Chama cha Afro-Shirazi
kilichoungwa mkono na Waafrika na
kile cha Zanzibar Nationalist Party kilichoungwa mkono na Wakoloni, Sultani
pamoja na jamii ya Waarabu. Chama cha ZNP baada ya kushindwa uchaguzi,
kilianzishakampeni za kushawishi wenye mashamba na mabepari wengine wenye
kumiliki njia kuu za uchumi, kuwafukuza kazi au kutowaajiri wafuasi wa ASP.
Halikadhalika, Chama cha ZNP kiliwatafutia kazi na kuwabakisha mashambani
Waafrika wote waliokubali kukiunga mkono. Wakati wa mvutano huo wa kisiasa kati
ya ASP na ZNP ikipamba moto, kulijitokeza tofauti miongoni mwa viongozi wa ASP.
Tofauti hizo zilichangiwa na uroho
wa madaraka, ubinafsi na kutokuwa na msimamo imara miongoni mwa baadhi ya
viongozi wa
chama hicho. Halikadhalika Serikali
ya Sultani nayo ilichochea migogoro hiyo ili ijinufaishe kisiasa. Migogoro hiyo
ilipelekea kujitoa
kwa baadhi ya Viongozi wa ASP ambao
walifanya mkutano na baadhi ya wanasiasa mashuhuri wa ASP huko Pemba Novemba,
1959 na kukubaliana kuanzisha Chama
kipya cha siasa cha Zanzibar and Pemba People’s Party.
(ZPPP) na Sheikh Muhammed Shamte kuwa
Mwenyekiti. Wakati vyama vya ASP, ZNP na ZPPP vikiwa katika malumbano makali ya
kisiasa, Serikali ya Kikoloni ilifanya matayarisho ya uchaguzi wa pili. Uchaguzi
ulifanyika tarehe 16 Januari, 1961 na siku moja kabla ya uchaguzi huo Serikali
ilitangaza kuwa chama kitakachoshinda kitaunda Serikali na Wizara zote zitakuwa
chini yake. Katika uchaguzi huo ASP ilishinda kwa kupata viti 10, ZNP kilipata
viti 9 na chama cha ZPPP kilipata viti 3. Kutokana na kuenea kwa chuki za
kisiasa miongoni mwa Wazanzibari, Vyama vikuu vya kisiasa vilifikia muafaka wa
kumaliza hali hiyo.Hatahivyo,ASP haikufikisha zaidi ya nusu ya kura na hivyo
haikuweza kuunda Serikali.Hivyo njia pekee iliyobakia ilikuwa ni kuishauri ZPPP
ichanganye viti vyake na chama kimoja kati ya ASP na ZNP. ZPPP na ZNP
viliungana. Hatahivyo, iliamuliwa kuwa iundwe Serikali ya muda na kusubiri
uchaguzi mwingine uliopangwa kufanyika mwezi Juni,1961. Waingereza walitoa
uhuru kwa Serikali ya Mseto ya ZNP/ZPPP ya Waziri Mkuu Muhammed Shamte. Chini
ya ushauri wa Waingereza, Shamte aliwatenga ndani ya Serikali yake baadhi ya viongozi
wa ZNP wenye msimamo wa Kikomunisti wakiongozwa na Abdulrahaman Babu, na hivyo kutokea
kutofautiana kwa baadhi ya viongozi wa ZNP na Serikali ya ZNP/ZPPP. Baada ya
kutengwa na Serikali hiyo walijitoa ZNP na kuanzisha Chama cha Umma. Chama hicho
kilivunjwa mara tu baada ya Mapinduzi ya mwaka 1964 na hapo viongozi na wafuasi
wake walijiunga na Serikali ya ASP chini ya uongozi wa Abeid Karume.
Zanzibar ilikuwa na wakati mgumu
katika kupigania uhuru.Waingereza walijikita zaidi kwa madhumuni ya kibiashara
na kwa nia ya kukomesha biashara ya utumwa. Hii ilikuwa ni kwasababu,walitaka
nguvu kazi rahisi ambayo ilikuwa inapotea kwa kufanywa watumwa kwa uzalishaji
wa malighafi kwa ajili ya viwanda vyao.Ulaya, halikadhalika kutokana na Mapinduzi
ya Viwanda Ulaya yalisababisha Waingereza kuja kutafuta soko kwa ajili ya
bidhaa zao.Waingereza walifikia makubaliano na Sultani mwaka 1822 ili
kukomesha biashara ya utumwa, lakini
ilichukua zaidi ya miaka 50 hadi utumwa kutokomezwa. Makubaliano ya Waingereza
na Wajerumani ya mwaka 1890 yalifanya Zanzibar kuwa koloni la Waingereza ambao
walimshirikisha Sultani katika utawala wao. Waingereza waliainzisha ubaguzi wa
rangi Zanzibar kwa Wazungu na Waarabu kupendelewa kuwa tabaka la juu na
Waafrika la chini.Waingereza walifanya Zanzibar kuwa ni koloni la Waarabu na ilipofika
Desemba 1963, Sultani alipewa mamlaka kamili ya kutawala Zanzibar. Tarehe 12
Januari 1964, aliyekuwa Sultani wa Zanzibar,Jamshid bin Abdulla, aling’olewa madarakani
katika Mapinduzi yaliyokuwa yameandaliwa kwa usiri, ustadi na ujasiri mkubwa wa
Wanamapinduzi wa Afro-Shirazi Party (ASP) na Jamhuri ikatangazwa.
Muundo wa Muungano wa Tanzania kama
ulivyoelezwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, una vyombo
viwili vyenye mamlaka ya utendaji ambavyo ni Serikali ya Jamhuri ya Muungano na
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Vyombo viwili vyenye mamlaka ya kutekeleza
utoaji haki ambavyo ni Mahakama ya Jamhuri ya Muungano na Mahakama ya Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar; na vyombo viwili vyenye mamlaka ya kutunga sheria na
kusimamia utekelezaji wa shughuli za umma ambavyo ni Bunge na Baraza la Wawakilishi.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inashughulikia mambo yote ya
Muungano kama yalivyoainishwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
ya mwaka 1977 na yasiyo ya Muungano kwa upande wa Tanzania Bara na Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar
inayoshughulikia mambo yote yasiyo ya Muungano kwa upande wa Tanzania Zanzibar.Muungano
wa Tanzania ni tukio la nadharia iliyotafsiriwa katika
vitendo, kwani kuunganisha
Tanganyika na Zanzibar ilikuwa ni hatua ya watu walio wakweli. Ni ushahidi
unaojitosheleza kuwa wananchi wa Tanganyika na wa Zanzibar wakiongozwa na
viongozi wao wa mapambano ya kudai uhuru, walitoa kauli zilizokuwa zikimaanisha
walichofikiri na kuazimia na wala
siyo kwa sababu ya kusombwa na jazba za kisiasa.
SABABU
ZA KUWEPO KWA MUUNGANO
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar
umekuwepo kutokana na
sababu zifuatazo:-
1.
Kuwepo kwa mahusiano ya karibu
kihistoria baina ya Tanganyika na Zanzibar katika nyanja mbalimbali kama vile udugu
wa damu, biashara, utamaduni, lugha na mahusiano ya karibu kisiasa hususani
baina ya TANU na ASP.
2.
Moyo wa kuwa na Muungano wa Afrika
hususan kwa kuanziana Shirikisho la Afrika Mashariki. Hata kabla ya uhuru wa Tanganyika,
Mwalimu Nyerere pamoja na viongozi wengine waliokuwa wakipigania utaifa katika
ukanda wa Afrika Masharikiwalikuwa na matarajio ya kuwa na Muungano wa Afrika.Mwalimu
Nyerere binafsi alipendelea uwepo Muungano wa Afrika kwa kuanzia na
Mashirikisho ya kikanda. Baada ya kushauriana na viongozi mbalimbali wa
iliyokuwa Jumuiya ya Wapigania Uhuru wa Afrika Mashariki na Kati (Pan- African Freedom
Movement for East and Central Africa - PAFMECA) Mwalimu Nyerere alitoa tamko
wakati wa mkutano wa nchi huru za Afrika uliofanyika Addis Ababa mwaka 1960
kwamba; “Wengi wetu tunakubaliana bila kikwazo kwamba Shirikisho la Afrika
Mashariki litakuwa ni jambo zuri. Tumesema na ni kweli kwamba mipaka
inayotenganisha nchi zetu imewekwa na mabeberu na sio sisi wenyewe na kwamba
tusikubali itumike dhidi ya umoja wetu...lazima tuzisumbue ofisi za wakoloni
kwa nia si ya kudai uhuru wa Tanganyika, kisha Kenya, na Uganda halafu Zanzibar
lakini kwa nia ya kutaka uhuru wa Afrika Mashariki kama Muungano mmoja wa
Kisiasa”.(imeripotiwa kwenye gazeti la Tanganyika Standard, Novemba 1964) Mapinduzi
ya Zanzibar mnamo mwezi Januari, 1964 yalifanyika wakati Mwalimu Nyerere akiwa
ameshachoshwa na kukatishwa tamaa na mazungumzo ya Shirikisho la Afrika
Mashariki.Mapinduzi haya yaliiweka madarakani Serikali ya chama cha ASP
kilichokuwa na mahusiano ya karibu na TANU kwa upande wa Tanganyika. Kwa
uhakika zaidi, upo mchanganyiko wa sababu mbalimbali za Muungano huu kama vile
historia za nchi hizi mbili, ukaribu wa nchi hizi mbili, muingiliano wa
kijamii, ushirikiano wa kibiashara, ushirikiano madhubuti na wa muda mrefu wa
kisiasa baina ya TANU na ASP, ushirikiano na urafiki wa muda mrefu kati ya
watu, viongozi, na wakati wa harakati za utaifa uliopelekea uhuru wa nchi hizo
mbili, sababu za kiusalama n.k.
HATI
YA MAKUBALIANO YA MUUNGANO
Msingi wa Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 ni Hati
za Muungano za mwaka 1964. Hati za Muungano zilitiwa saini na waasisi wa Muungano
tarehe 22 Aprili, 1964, na hapo Tanganyika na Zanzibar kuwa dola moja, ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Mapatano ya Muungano
yaliunganisha mataifa mawili yaani Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya watu wa
Zanzibar na kuweka Taifa moja la Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar
kwa misingi ya Katiba na misingi inayotambulika Kimataifa.Jina la Jamhuri ya
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar lilibadilishwa baadae na kuwa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania.Baada ya Muungano, Mwalimu J. K. Nyerere alikuwa Rais wa kwanza
na Sheikh Abeid Amani Karume, alikuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.Tarehe 26 Aprili, 1964 Bunge la Tanganyika lilipitisha Sheria za Muungano.
Halikadhalika Sheria hizi zilithibitishwa na Baraza la Mapinduzi Zanzibar.
Sheria hizi za Muungano zilithibitisha Hati za Muungano, zilitaja Rais na
Makamu wa Rais, zilitaja Muundo wa Muungano na Katiba ya Muungano. Mnamo tarehe
27 Aprili 1964,waasisi wa Muungano walibadilishana Hati za Muungano na wajumbe
saba (7) wa Baraza la Mapinduzi waliapishwa kuwaWabunge wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao ni: Sheikh Abeid Amani Karume, Bw.
Kassim Abdala Hanga, Bw. Abdulrahaman Mohamed Babu, Sheikh Hassan Nassor Moyo,
Sheikh Aboud Jumbe, Sheikh Hasnu Makame na Sheikh Idris
Abdul Wakil. Wote hawa walifanya
Mawaziri wa Serikali ya Muungano. Kati ya Viongozi hawa wawili wako hai hadi
sasa. Nao ni Aboud Jumbe na Hassan Nassor Moyo.
Kabla ya siku ya Muungano, kulikuwa
na Katiba mbili; Katiba ya Tanganyika ya mwaka 1962 na upande wa Zanzibar
kulikuwa na Amri za Katiba (Constitution decrees). Katiba ya Tanganyika baada ya
kufanyiwa marekebisho iliendelea kutumika kama Katiba ya
Muungano wakati ule wa mpito,
kuanzia tulipoungana hadi ilipopitishwa Katiba ya Muungano kwa mujibu wa
Makubaliano ya Muungano na Sheria za Muungano. Aidha, marekebisho hayo yalimtaja
Rais wa Zanzibar kuwa ni Makamu wa kwanza wa Rais,
akiwa ni msaidizi wa Rais kwa
masuala yote ya kiutawala kwa upande wa Zanzibar, na Waziri Mkuu kuwa ni Makamu
wa Pili wa Rais ambaye atamsaidia Rais kwa masuala yahusuyo upande wa Tanganyika
na kiongozi wa shughuli za Serikali Bungeni. Katiba ya muda ya mwaka 1965 ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliainisha mambo kumi na moja (11) ambayo
yalikubalika kuwa ni ya Muungano chini ya usimamizi wa Serikali ya Muungano.Mambo
hayo ni;
Ø Katiba na Serikali ya Muungano
Ø Mambo ya Nchi za Nje
Ø Ulinzi
Ø Polisi
Ø Mamlaka juu ya mambo yanohusika na hali ya hatari
Ø Uraia
Ø Uhamiaji
Ø Mikopo na Biashara ya Nchi za Nje
Ø Utumishi katka Serikali ya Jamhuri ya Muungano
Ø Kodi ya Mapato inayolipwa na watu binafsi na mashirika,ushuru
wa forodha na ushuru wa bidhaa zinazotengenezwanchini Tanzania unaosimamiwa na
Idara ya Forodha.
Ø Bandari mambo yanayohusika na usafiri wa anga, posta nasimu.
Katiba ya muda ya mwaka 1965
ilianiainisha utawala wa Serikali yamfumo wa chama kimoja, TANU kwa Bara na ASP
kwa Zanzibar.Katiba hii, ilizingatia misingi ya Makubaliano ya Muungano ya
mwaka 1964 na Sheria za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Katiba ya
muda ya mwaka 1965 iliainisha
Serikali mbili, Uwakilishi wa Zanzibar katika Bunge la Muungano na uongozi wa
Serikali ya Zanzibar.Serikali ya Muungano ikiwa na mamlaka juu ya mambo yote ya
Muungano na mambo yote yasiyo ya Muungano kwa upande wa
Tanganyika. Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar ikiwa na mamlaka juu ya mambo yote yasiyo ya Muungano yahusuyo
Zanzibar.
0 comments:
Post a Comment